Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge, ametembelea na kukagua Mradi wa barabara ya Kwala-Vigwaza inayojengwa kwa kiwango cha Zege yenye urefu wa km.15.5 ambao utagharimu sh. bilioni 36 na kuunganisha mradi mkubwa wa Kimkakati wa Bandari kavu Kwala.
Barabara hiyo ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 54.1 itnapunguza athari zitokanazo na kupitisha malori mazito ambayo hupelekea matengenezo ya mara kwa mara na kutumia gharama kubwa kila wakati.
Barabara hiyo ambayo ni mkombozi kwa vijiji vya Vigwaza, Mnindi na Kwala itarahisisha shughuli za uchukuzi kati ya bandari na barabara Kuu ya Morogoro.
Akitembelea mradi huo pamoja na kujionea Hali ya ujenzi wa bandari kavu ya Kwala, Kunenge alieleza kuwa ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji maelekezo waliyopewa na Katibu Mkuu Kiongozi wiki kadhaa zilizopita wakati alipofika eneo hilo na kuwataka kuhakikisha kuwa barabara na bandari hiyo iwe imeanza kazi ndani ya Miezi mitatu.
"Mradi huu unakwenda katika maeneo makubwa ya uwekezaji Kongani ambayo itajengwa viwanda 300-350 ,Bandari Kavu, maeneo ya kubadilisha vichwa vya treni, hivyo tunampongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kutimiza ahadi yake kuwa atatekeleza na kumaliza miradi iliyoanza tangu kipindi cha awamu ya tano na kuanzisha miradi mipya Kama huo wa Kongani ya uwekezaji wa viwanda.” Alisema Kunenge.
Kunenge alielekeza jitihada kuongezeka ili kuhakikisha kuwa ndani ya miezi mitatu barabara ya zege na bandari iwe imekamilika na kuanza kutoa huduma.
“Lakini tunafahamu pia itaendelezwa kujengwa barabara nyingine ya njia mbili, Kazi yetu ni kusimamia na kuhakikisha miradi hii inajengwa kwa viwango vinavyotakiwa na kukamilika kwa wakati kwa manufaa ya wananchi na Taifa." Alisisitiza RC Kunenge na akaongeza kuwa hilo ni eneo la kimkakati, amabalo mataifa ya Burundi, Uganda na Rwanda watakuwa na eneo la kuhifadhi mizigo yao na linazunguka viwanda, litarahisisha kusafirisha mizigo yao, patakuwa na reli ya SGR, barabara na EPZA."
Mkuu huyo wa mkoa alibainisha kuwa wapo nyuma ya Rais kusimamia miradi yote na eneo la uwekezaji kwani Rais ametembea falme za Kiarabu, Dubai, Ufaransa, Marekani kutafuta wawekezaji na kuitangaza nchi hivyo matarajio ya watanzania ni kupata wawekezaji wengi na mkoa upo vizuri.
Awali msimamizi wa mradi wa barabara hiyo, Jacob Mambo alisema mradi huo ulianza Novemba 2020, wakati ambao Mamlaka ya Bandari (TPA) ilimpatia Wakala wa barabara Tanzania TANROADS jukumu la kusimamia ujenzi wa barabara hii Kama Mhandisi Mshauri kupitia kitengo Cha TECU Mkoa wa Pwani.
Mambo alifafanua hali ya ujenzi na kusema kuwa matabaka ya chini yameshafikia zaidi ya asilimia 90 ya kazi, tabaka lililoimarishwa kwa saruji limejengwa kwa asilimia 81.29, makaravati ya kupitisha maji asilimia 96.3 na madaraja makubwa matatu kwa asilimia 100.
Mambo alieleza kuwa tabaka la zege limefikia asilimia 40 ambapo jumla ya mradi umefikia asilimia 54.1 na utakamilika baada ya miezi miwili na nusu.
Alisema kulikuwa na changamoto ndogondogo lakini Serikali na TPA wameshamaliza na mkandarasi kishalipwa asilimia 33 na mradi ni wa Bilioni 36.
Kwa upande wake Alexander Ndibalema kutoka TPA alieleza kati ya heka 502, wameshazungusha uzio heka 60 kwenye eneo la urefu wa km.2.96 ,heka 5 wameziendeleza kwa ajili ya Bandari na kazi imefanywa na Suma JKT.
Ndibalema alisema ujenzi unaenda Sambamba na ujenzi wa barabara kwa Ajili ya uingizaji mizigo itakayofika bandari ya Kwala itakuwa inakwenda kwa njia ya reli na ujenzi umefikia asilimia 65 na utakamilika kwa miezi miwili na nusu.mo
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.