Mradi wa ujenzi wa Daraja jipya la WAMI lenye urefu wa mita 510 na upana wa mita 11.85 linalojengwa umbali wa mita 670 pembeni mwa daraja la zamani linatarajiwa kuanza kutumika Mwezi Julai 2022.
Mradi huo ambao ni moja ya Miradi ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa Mkoani Pwani umefikia asilimia 91 huku upande wa barabara unganishi ukiwa umefikia asilimia 79.5.
Hayo yamebainika Mei 23 wakati Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alipofanya ziara ya ukaguzi katika baadhi ya miradi ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa Mkoani Pwani ambayo yote ipo katika hatua nzuri za uendelezaji na akasema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo na kuhakikisha kuwa inakamilika ili itoe huduma kwa wananchi.
Kunenge alifafanua kuwa mradi huu ni tunu ya mkoa na Taifa na utagharimu zaidi ya sh. bilioni 75.134 bila VAT na kuwa daraja la WAMI la zamani lilijengwa 1959 na ni kiungo kutoka Chalinze kwenda mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania na nchi jirani.
"Daraja lile la zamani halikidhi mahitaji ya magari yanayopita kwa kuwa lilijengwa miaka mingi iliyopita na ni jembamba lenye njia moja, barabara zinazounganisha daraja hili ziko kwenye miinuko mikali na kona mbaya ambapo ajali mbaya na vifo vimekuwa vikitokea mara kwa mara, hivyo hili jipya likikamilika litakuwa Mkombozi." alisema Kunenge.
Aliongeza kuwa baada ya mkandarasi kukamilisha ujenzi huo atafanya ukarabati wa Daraja la zamani ili nalo litoe huduma.
Vilevile Kunenge alikagua Mradi wa barabara ya Kwala -Vigwaza yenye urefu wa kilometa 15.5 inayounganisha barabara Kuu ya Morogoro kupita katika vijiji vya Vigwaza, Mnindi na Kwala ambayo kwa Sasa inajengwa kwa kiwango cha Zege ili kurahishisha shughuli za uchukuzi kati ya bandari na barabara Kuu ya Morogoro.
Awali mwakilishi wa Meneja wa Wakala wa barabara ( TANROADS ) Mkoa wa Pwani Evelyn Mlai alisema kuwa ujenzi wa barabara unganishi utakamilika Novemba mwaka huu ikiwa na urefu wa km. 3.8 inayojengwa kwa kiwango cha lami yenye njia mbili zenye Jumla ya upana wa mita 12 ambazo ni mita 3.5 kwa kila njia ipitishayo magari, mita 2 za bega la lami na mita 0.5 za bega lisilo la lami kila upande.
"Kampuni inayosimamia kazi za ujenzi ni ILSHIN Engineers,& consultant Co. Ltd toka Jamhuri ya Korea Kusini ikishirikiana na Advanced Engineering Solutions Limited ya Tanzania kwa gharama ya sh. bilioni 6.3 bila VAT." alisema Evelyn.
Evelyn alieleza kuwa mkandarasi alianza kazi Oktoba 22 mwaka 2018 na hadi sasa utekelezaji wa kazi umefikia asilimia 79.5 huku katika daraja sehemu ya chini utekelezaji wake umefikia asilimia 100 ikiwemo misingi na nguzo nne na kuta mbili za mwanzo na mwisho wa Daraja.
Nae Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainab Abdallah alibainisha kuwa daraja hilo litakuwa na uwezo mkubwa katika usafirishaji na kufungua milango ya kimaendeleo na kukuza uchumi wa nchi yetu.
Aliwaambia Wana Bagamoyo Mradi ukikamilika wautumie kama fursa kwao ili kujiongezea tija.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.