Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, amefungua mafunzo ya siku mbili kwa vikosi kazi vya utekelezaji wa Mfumo wa Fursa na Vikwazo kwa Maendeleo (O&OD) ulioboreshwa. Mafunzo hayo yanawahusisha wataalamu mbalimbali kutoka ngazi ya Mkoa na Halmashauri.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi hicho kilichofanyika Januari 15, 2026, katika ukumbi wa mikutano uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mnyema amewasisitiza wataalamu hao kusikiliza kwa umakini mafunzo hayo ili kuongeza ufanisi katika uingizaji wa kazi na taarifa sahihi, jambo litakalowezesha mkoa kutekeleza mfumo huo ipasavyo.
Ameeleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu na si ya mzaha, kwani yana lengo la kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa maslahi mapana ya wananchi. Ameongeza kuwa Mkoa wa Pwani unaendelea kufanya vizuri katika maeneo mbalimbali, hivyo ni wajibu wa wataalamu kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi bila visingizio.
“Baada ya mafunzo haya, nataka kuona mabadiliko yanayoonyesha mkoa unakwenda vipi. Haikubaliki kushindwa kutimiza majukumu yetu,” amesema Mnyema.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali inataka wananchi waone miradi yao ikitekelezwa kwa vitendo kulingana na vipaumbele walivyobainisha. Katika hilo, amewataka wataalamu kutoa taarifa sahihi na kuepuka tabia ya “kupika taarifa”. Pia amekumbusha kuwa utekelezaji wa mfumo wa O&OD unapaswa kuzingatia kauli mbiu ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inayosisitiza kutokukubali kushindwa.
“Maeneo yenye changamoto tumefundishwa twende tukayafanyie kazi. Mfumo huu unatusaidia kupanga na kutekeleza miradi kulingana na vipaumbele vya wananchi. Hapa tumekula kiapo cha uadilifu, hivyo yeyote atakayekiuka maelekezo na taratibu atawajibishwa kwa mujibu wa sheria,” amesisitiza Mnyema.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Pwani, Grace Tete, amesema baada ya mafunzo hayo mkoa unatarajia kuongeza kiwango cha utekelezaji wa Mfumo wa O&OD ulioboreshwa pamoja na kuwa na mipango bora ya bajeti inayozingatia mahitaji na jitihada za jamii.
Ameongeza kuwa awali mkoa ulikuwa unakabiliwa na changamoto ya uelewa mdogo wa mfumo huo, hususan kwa vikosi kazi vya ngazi ya mkoa na halmashauri kutofahamu kikamilifu viashiria vya O&OD ulioboreshwa vilivyowekwa katika Mfumo wa IMES na namna ya kuviingiza kwenye mfumo huo. Hata hivyo, amesema kupitia mafunzo hayo, mkoa unatarajia kufanya vizuri zaidi katika utekelezaji na ufuatiliaji wa mipango ya maendeleo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.