Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amewataka Makarani wa Sensa kuzingatia kanuni sheria na taratibu ili zoezi hilo lifikie malengo ya kupata takwimu sahihi.
Kunenge alitoa agizo hilo alipokuwa akifunga mafunzo ya siku 21 ya Makarani wa Sensa wapatao 211 kutoka Halmashauri zote za mkoa huo.
Kunenge alisema kuwa zoezi la sensa kwa nchi ndiyo kila kitu hivyo Makarani hao wanapaswa kwenda kuwafundisha kwa usahihi Makarani wa ngazi za wilaya za mkoa huo.
"Mnapotoa mafunzo kwa Makarani mnapaswa kuzingatia taratibu na kanuni za sensa mlizofundishwa kwa usahihi na ufasaha,"alisema Kunenge.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sara Msafiri alisema kuwa Makarani hao wamepewa dhamana kubwa na nchi na wajitoe kizalendo kwa ajili ya nchi yao hata kama zitatokea changamoto mbalimbali kwani zoezi likiharibika leo ni hasara kwa miaka 10 ijayo.
Msafiri alisema kuwa baadhi ya maeneo kumekuwa na changamoto za maendeleo kutokana na baadhi ya waliohusika na sensa zilizopita kwa kutotoa takwimu sahihi hivyo rasilimali kuonekana hazitoshelezi
Kwa upande wake mratibu wa sensa mkoa wa Pwani Adela Temba alisema kuwa Makarani hao wa sensa wote wamefaulu baada ya kufanya mitihani ambapo ufaulu ni asilimia 74.
Temba alisema kuwa jeshi hilo limefaulu vizuri na wana imani watafanya vizuri na wamefikia viwango lengo ni kufanya zoezi hilo kuwa la kisasa na mafanikio ambapo zoezi hilo litafanyika Agosti 23 mwaka huu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.