Uongozi wa Mkoa wa Pwani, ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Abubakar Kunenge, leo Desemba 24, 2025, umekutana na ugeni kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Mussa Makame, kwa lengo la kujadili utekelezaji wa mradi wa bomba la gesi kutoka Kinyerezi hadi Chalinze.
Akizungumza katika kikao hicho kifupi kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Kunenge amesema mradi huo ni miongoni mwa jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuufanya Mkoa wa Pwani kuwa mkoa wa kimkakati kiuchumi.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo utachochea uwekezaji, hususan katika sekta ya viwanda, hali itakayoongeza uzalishaji, kuimarisha ajira na kukuza mapato ya Mkoa. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa ushirikiano wa karibu kati ya Mkoa wa Pwani na TPDC ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati uliopangwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame, amesema kuwa sasaShirika tayari limemaliza uanisha wa njia ya kupitisha bomba hilo huku akisema upembuzi yakinifu wa mradi huo utakamiika Aprili 2026, na kuongeza kuwa bomba la gesi litapita sambamba na njia za umeme chini ya usimamizi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Akiwasilisha taarifa ya kina ya mradi huo, Mhandisi Angelindile Marandu amesema kuwa gharama za utafutaji wa njia za kupitisha bomba, upembuzi yakinifu pamoja na tathmini ya athari za mradi kwa mazingira na jamii ni zaidi ya shilingi bilioni 2.3.
Aidha amesema Mradi utatekelezwa na kampuni ya Gulf Interstate Engineering kwa kushirikiana na Paulsam Geo-Engineering Co. Ltd. Ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 15 tangu tarehe ya kusainiwa kwa mkataba.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.