Mkoa wa Pwani unatarajia kuwapatia chanjo ya matone (POLIO) Watoto 200,967 waliochini ya miaka mitano ili kuwajengea kinga na kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa kampeni hiyo ni ya nyumba kwa nyumba na itafanyika kuanzia Mei 18 hadi 21, 2022 mkoani hapo.
Alibainisha kuwa watoto wote chini ya miaka mitano watapata chanjo hii bila kujali kama walishapata katika ratiba zao za kawaida za chanjo.
Kunenge aliitaka jamii itambue usalama wa chanjo hiyo na wasiingie katika upotoshaji wowote kwani ni Kama chanjo nyingine na akasisitiza kuwa ugonjwa huo hauna tiba ila hukingwa na chanjo ya Polio ambayo ipo katika mfumo wa matone.
"Nchi ya Malawi na Tanzania kuna mwingiliano mkubwa wa kibiashara na huduma nyingine za kijamii hivyo hatari ipo na chanjo ni muhimu itasaidia kuzuia ugonjwa huo usienee ". Alifafanua Kunenge.
Alibainisha kuwa ,chanjo ni ileile inayotumika miaka yote na lengo ni kuongeza kinga, kuzuia mlipuko na kudhibiti watoto wasipatwe na virusi vya ugonjwa huo.
Alieleza kuwa kwa mara ya mwisho Tanzania ilipata mgonjwa wa Polio Julai 1996 hivyo kampeni hii inatarajiwa kufanyika katika nchi zinazopakana na Malawi ikiwemo Zambia,Msumbuji na Zimbabwe.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Pwani amewataka wananchi wa mkoa huo na ajamii kwa ujumla kuipokea kampeni hii na kutokuwa na hofu kwani chanjo hiyo ni Salama.
Hatua hiyo imekuja kufuatia nchi ya Malawi kutoa tamko la kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa huo Februari 17 mwaka huu baada ya mtoto mmoja kutoka Mji Mkuu wa Lilongwe kuthibitika kuwa na ugonjwa huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.