Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo leo Aprili 13, 2021 ameendesha kikao cha siku Moja cha Wadau wa Vitambulisho vya Wajasiriamali wadogo Mkoani hapo.
Akizungumza kwenye ufunguzi kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano ofisini kwake Kibaha, Ndikilo amesema wamekutana ili kuweka Mikakati ya kuhakikisha wanatekeleza maelekezo ya Serikali ya kuwarasimisha Wafanyabiashara wadogo kwa kuwapatia Vitambulisho kwa malipo ya Shilingi 20,000. Ameeleeza kuwa utaratibu huo wa kuwatambua Wafanyabiashara wadogo ulianza mwaka 2019 ambapo Mkoa huo ulifanikiwa kugawa Vitambulisho 59,045 sawa na asilimia 98 ya Vitambulisho 60,000 na kukusanya Shilingi Bilioni 1.181. kwa mwaka 2020 Mkoa huo Uligawa Vitambulisho 17,607 sawa na Asilimia 27 ya Vitambulisho 63,500 vilivyotolewa na kukusanya Shilingi Milioni 337.1
Ameeleeza kuwa kwa Mwaka 2021 zoezi hilo limeanza Mwezi Machi 2021 ambapo Mkoa huo umepewa Vitambulisho 61,000, ameelekeza Viongozi wote Kwenda kusimamia Jukumu la Ugawaji Vitambulisho ili Malengo ya Serikali ya Urasimishaji wa Biashara na kuwezesha Serikali kupata mapato kwa ajili ya kuhudumia Wanachi yatimie.
Amewataka Viongozi na Watendaji Mkoani hapo kuhakikisha wanaongeza kasi ya uuzaji Vitambulisho hivyo, ambapo kwa mwaka huu 2021 zoezi hilo litafanyika Kupitia mfumo wa Kielektroniki Machinga Online Registration System
Katika kuhakikisha wanaongeza kasi ya uuzaji Vitambulisho hivyo Ndikilo amewaelekeza Viongozi hao mambo yafuatayo:- kuongeza nguvu kwenye utoaji wa Elimu kwa Wafanyabiashara wadogo, amewataka Watendaji katika ngazi ya Kata na Vijiji kupeana malengo maalumu ya kuhamasisha utoaji wa Vitambulisho, amewataka kuweka utaratibu wa kuwafikia Wafanyabiashara Wadogo na Watoa huduma kwenye maeneo yao badala ya kuwasubiri maofisini.
Amewataka kupitia kikao hicho kuweka Agizo la Wafanyabiashara Wadogo kwenye masoko na Minada kutoruhusiwa kufanya Biashara kwenye maeneo hayo bila ya Vitambulisho na kuwataka Wakurugenzi Kufanya Ukaguzi katika masoko na minada ili kufuatilia Maagizo hayo.
Amewataka pia Viongozi wa Wafanyabiashara Mkoani hapo TCCIA, Jumuiya ya Wafanyabiashara, Shirika la Wamachinga kushirikiana na Serikali ya Wilaya na Mkoa katika kuhamasisha uchukuaji wa Vitambulisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.