Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge ameridhishwa na maandalizi ya timu ya UMITASHUMTA Mkoani humo kushiriki katika michezo hiyo kitaifa inayotarajiwa kufanyika Mkoani Tabora kuanzia Julai 30 hadi Agosti nane 2022.
Mhe. Kunenge amebainisha hayo Julai 24, wakati akifunga michezo hiyo uliyodumu kwa muda wa siku tatu kuanzia Julai 22 hadi 24, 2022 kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Kibaha na kuona utayari wa wanamichezo wa Mkoa huo kuibuka na ushindi .
“Kwa haya maandalizi, na utayari mlionao wa kupambana kuuletea heshima Mkoa wetu na hatimae nchi yetu, mimi ninachukua ulezi wa vijana hawa,” alisema Kunenge.
Alisema mikakati mingi ya kimaendeleo Mkoani humo ikiwemo ya viwanda imefanikiwa hivyo akaelekeza mikakati hiyo iimarishwe kwenye michezo kwani mkoa huo unao vijana wengi wenye vipaji ambavyo vinapaswa kuendelezwa.
"Waziri wa Michezo Mohamed Mchengerwa anatoka mkoa wa Pwani hivyo lazima tuonyeshe uwezo ili kumuunga mkono kwa Mkoa wetu kuwa na hamasa kubwa ya michezo," alisema Kunenge.
Akizungumzia wimbo ulioimbwa na mwanafunzi Dotnata Athumani kutoka Kisarawe wa kuhamasisha watu kushiriki kwenye Sensa ya Watu na makazi itakayofanyika Agosti 23, 2022, RC kunenge ameusifu akisema kuwa mwanafunzi huyo ameutendea haki kwani ameuimba vizuri ukiwa na fani, maudhui na ujumbe mzuri.
Naye Afisa Elimu Mkoa wa Pwani Sarah Mlaki akitoa taarifa ya awali alisema kuwa mashindano hayo ni ya 26 na kuwa yamefanyika kwa siku tatu kuanzia Julai 22 hadi leo Julai 24, 2022 yakijumuisha Wanafunzi 900 na Walimu 61.
“Katika Mkoa wa Pwani kuna Shule mbili maalum za Michezo ambazo ni Zuhuwale ya Kibaha na Fukayosi iliyopo Bagamoyo, lakini kutokana na uhotaji tumeamua kufanya Uteuzi wa shule zingine mbili ili kukidhi mahitaji,” alisema Mlaki.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.