Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ametoa maelekezo kwa Halmashauri za Mkoa huo kuibua vyanzo vipya vya mapato ambavyo vitasaidia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo
Pia Kunenge ameziagiza kuongeza umahiri wa kukusanya mapato sambamba na kuwa makini kwenye matumizi kwa kutumia maeneo yenye tija.
Kunenge ameyasema hayo kwa nyakati tofauti leo Juni 25, 2024 alipohudhuria vikao vya mabaraza maalumu ya Halmashauri za Waya ya Kibaha na Chalinze kwa ajili ya kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
Akizungumza katika vikao hivyo Kunenge alisema kwasasa Halmashauri hizo zinatakiwakujikita kutengeneza mapato kwa kuzingatia kuweka miikakati ya kuibua vyanzo vipya na kuvifanya vikue na kuwa endelevu.
"Fursa mnazo na mnafanya vizuri lakini mnaweza kufanya vizuri zaidi ya hapo, kinachotakiwa sio tu asilimia ya makusanyo ya lengo (bajeti), bali ni kiasi gani unapata ili kuwaletea wananchi maendeleo," amesema
Amewasisitiza madiwani na watendaji katika Halmashauri hizo kufikiria wanaweza kufanya ili kuzisaidia kutoa huduma kwa wananchi.
"Changamoto na mahitaji ya wananchi yanakuwa yakiongezeka kila siku hivyo mnatakiwa kuongeza uwigo makusanyo ya mapato" amesema kunenge.
Kadhalika Kunenge amewaasa kutoridhika na hali hiyo kwa kuwa bado kuna mahitaji makubwa ya huduma kwa wananchi kwani kila mwaka malengo yanaongezeka kutokana na idadi ya watu kuongezeka.
"Watoto wanazidi kuzaliwa, kuna mahitaji kama madarasa, vituo vya kutolea huduma za afya, mahitaji ya maji, miundombinu, haya yote yanahitaji mapato hivyo wekeni jitihada na mikakati ya kuongeza ukusanyaji," amesema.
Katika mikutano hiyo, Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta mbali na kuzipongeza Halmshauri hizo kwa kupata hati safi na kwa kuvuka lengo la makusanyo, amezielekeza kumaliza hoja zilizobaki.
Mchatta pia amezelekeza Halmashauri hizo kutekeleza maagizo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kutumia vitendea kazi kama vile vishikwambi na matumizi ya mifumo kama ule wa e-office na mingine ili kuondokana na matumizi ya karatasi.
Naye Mkaguzi wa nje Mkoa wa Pwani toka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi CPA Pastory Masawe amezipongeza Halmashauri hizo kwa kupata hati safi na akatahadharisha kutobweteka na kuharibu hiyo sifa walizonazo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.