Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo, amewaagiza wakuu wa Wilaya Mkoani humo kuhakikisha kuwa ujenzi wa vyumba vya madarasa ya Sekondari unakamilika kabla ya Januari 31, 2018ili kuwezesha wanafunzi waliofaulu mtihani wa darasa la saba kujiunga na kidato cha kwanza.
Mhandisi Ndikilo ametoa agizo hilo wakati wa ufunguzi wa kikao cha chaguzi za shule kwa wanafunzi kutoka shule za msingi za mkoa wa Pwani waliofaulu mtihani wa darasa la saba wanaopaswa kujiunga na elimu ya sekondari kidato cha kwanza.
Katika kikao hicho kilichowajumuisha wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa, Wabunge, wakuu wa shule na wadau wengine wa elimu mkoa wa Pwani, Mhandisi Ndikilo ametumia fursa hiyo kueleza kuwa suala la kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na miundo mbinu mingine katika shule inapaswa kufanywa kwa ushirikiano wa Viongozi wote na wadau wa elimu ili wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari waweze kupata nafasi.
“Nendeni mkatekeleze maelekezo haya ili wanafunzi waliokosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2019 katika chaguo la kwanza kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa waweze kuchaguliwa na kuanza masomo katika awamu ya pili mwezi Februari” amesisitiza mhandisi ndikilo.
Mhandisi Ndikilo amewataka wakuu wa Wilaya kwenda kukaa na watendaji wao wanaohusika na maswala ya elimu kutafuta ufumbuzi wa kuzisaidia shule zilizofanya vibaya kwenye matokeo ya mitihani ya taifa ya darasa la saba ili kuhakikisha kuwa hazirudii kupata matokea hafifu katika mitihani hiyo ijayo.
Kuhusu kudhibiti suala la mimba kwa wnafunzi mashuleni, Mhandisi Ndikilo amewaagiza Wakuu wa Wilaya kuchukua hatua kwa wale wote ambao wamewapa mimba wanafunzi na kusababisha wakatishe masomo yao.
“Hakikisheni kuwa wahusika wanakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria “ amesema Mhandisi Ndikilo na kuongeza kuwa “natoa rai kwa viongozi wa Serikali za mitaa na watendaji wote kuhakikisha kuwa yeyote yule atakaejihusisha na vitendo vya kumaliza kesi za wanafunzi wanaopewa mimba mashuleni kwenye maeneo yao, nao wakamatwe na kuchukuliwa hatua kali za kisheria”.
Mkoa wa Pwani umefanya uchaguzi wa jumla ya wanafunzi 23,270 waliofaulu masomo ya elimu ya msingi kujiunga na elimu ya sekondari kidato cha kwanza ambapo kati yao wavulana ni 10,835 na wasichana ni 12,335. Ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 66.9 mwaka 2017 hadi kufikia asilia 77.79 mwaka huu na kuuwezesha Mkoa kushika nafasi ya 11 kitaifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.