Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema katika kipindi cha miaka mitatu mkoa huo umepokea kiasi cha sh. Trilion 1.19 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema fedha hizo zimetumika kutekeleza miradi ya afya, elimu, maji na miundombinu na hivyo kupunguza vikwazo vilivyokuwa vinakwamisha maendeleo kwa wananchi.
Amebainisha hayo leo Novemba 3, 2023 wakati akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari uliofanyika mjini Kibaha ulioandaliwa na ofisi yake kwa kushirikiana na ofisi ya msemaji mkuu wa serikali na kuhusisha viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa huo Abubakar Kunenge, kamati ya siasa ya CCM mkoa na Wilaya ya Kibaha, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa sehemu na vitengo Mkoa pamoja na wakuu wa taasisi za serikali ambao walielezea miradi iliyotekelezwa.
Kuhusu Miradi ya miundombinu ya barabara, amesema serikali ipo mbioni kuanza ujenzi wa upanuzi wa barabara kuanzia Dar es Salaam - Chalinze - Morogoro ambayo itakwenda kuondoa msongamano .
Aidha Kunenge amefafanua kuwa ujenzi wa barabara ya Chalinze-Utete ambayo itafungua milango ya kiuchumi na maendeleo katika maeneo hayo.
Katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, amesema viongozi wa Serikali wanatakiwa kuelezea miradi waliyoitekeleza ili kuondoa pengo kati ya wanachokiona Wananchi na kinachofanywa.
Ili kukabiliana na hali hiyo, amesema ni jukumu la viongozi na watendaji kueleza makubwa yanayofanywa na Serikali kwa wananchi kupitia mikutano mbalimbali.
Matinyi amesema, Serikali imekuwa ikipeleka fedha nyingi za miradi ya Maendeleo ya wananchi lakini hawaelezwi mchanganuo wa namna inavyotekelezwa ili kujua namna uongozi wao unavyowasaidia.
"Viongozi wa mikoa wanatakiwa kusimamia fedha za utekelezaji wa miradi hiyo ili iweze kuleta matokeo chanya kwa wananchi sambamba na kuwashirikisha kwa kila hatua kwenye maeneo husika," amesema.
Akielezea kuhusu mkutano huo amesema ni moja ya mpango uliozinduliwa hivi karibuni Jijini Dodoma kuwezesha viongozi kuelezea utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyofanywa na Serikaii kwa kipindi cha miaka mitatu na itaendelea katika mikoa yote 26 ya Tanzania bara ili taarifa za Serikali ziwafikie wananchi.
Katika mkutano huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti Hemed Magaro ameishukuru Serikali kwa namna ilivyotoa fedha za miradi ambayo imekwenda kutatua vikwazo kwa wananchi hususani katika eneo la delta.
"Awali wananchi wa Mbwera walikuwa wanasafiri km 90 kwenda kupata huduma za afya na wakati wa mvua walikuwa hawawezi kusafiri, hivyo ujenzi wa kituo cha afya katika eneo lao umeondoa tatizo lililokuwa linawakabili," ameeleza.
Kadhalika Kaimu Mkurugenzi wa wilaya ya Kisarawe, Deogratius Lukomanya, amesema kipindi cha miaka mitatu, Idara ya Elimu Msingi imefanikiwa kufikisha madarasa 616 kutoka 375 yaliyokuwepo na imejenga matundu 200 ya vyoo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.